Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa usimamizi madhubuti na utekelezaji wenye mafanikio wa mradi wa kielelezo wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, unaogharimu takribani shilingi bilioni 280.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo, kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuchochea ajira zaidi ya 30,000 katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi nchini, hatua inayotarajiwa kuimarisha uchumi wa buluu na kuongeza tija kwa wavuvi wa Kitanzania.
Pongezi kutoka Kamati ya Bajeti
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mashimba Ndaki, aliipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa maono ya Serikali katika sekta ya uvuvi.
Mhe. Ndaki alitoa pongezi hizo wakati wa kikao cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko pamoja na mpango wa ununuzi wa Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu kilichofanyika jijini Dodoma Mei 06, 2026.
“Niwapongeze Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kusukuma mbele mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko. Ni muhimu kuhakikisha bandari hii haitakuwa mradi mkubwa usiotumika. Tunahitaji pia kuharakisha ununuzi wa meli ili kuiwezesha kufanya kazi kikamilifu na kuepuka kuwa ‘white elephant’,” alisema Mhe. Ndaki.
Ushauri kuhusu Ununuzi wa MeliKuhusu mpango wa ununuzi wa Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu, Kamati hiyo imeishauri Serikali kuanza kujitegemea kwa kununua meli zake moja kwa moja badala ya kutegemea wafadhili, ambao mara nyingi wamekuwa wakichelewesha utekelezaji kutokana na masharti yao mbalimbali.
Maendeleo ya Mradi wa Bandari
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, aliieleza Kamati kuwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko umefikia asilimia 97, na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Mei 30, 2026.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa mpya katika sekta ya uvuvi, kuongeza ajira, na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa buluu nchini.
Shukrani kwa Kamati ya BajetiDkt. Bashiru aliishukuru Kamati ya Bajeti kwa ushirikiano na ushauri wanaotoa katika kusimamia miradi ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa bandari, ununuzi wa meli, ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki, pamoja na boti za kisasa za uvuvi.
Amesema mchango wa Kamati hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni