Breaking


Jumanne, 5 Mei 2026

RAIS WA KENYA, MHE. RUTO AHUTUBIA BUNGE LA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA: ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO KWA MATAIFA HAYA MAWILI

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Samoei Ruto, ameandika historia leo Mei 5, 2026 jijini Dodoma kwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, akisisitiza kuimarishwa kwa umoja, ushirikiano wa kikanda, biashara na maendeleo ya pamoja kati ya nchi za Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake iliyopokelewa kwa shangwe na wabunge, Mhe. Rais William Ruto alieleza kuwa Kenya na Tanzania zina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akihimiza kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa haya mawili na kupambana  na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na umaskini ili kujiletea maendeleo endelevu yenye manufaa ya watanzania na wakenya.

 “Ushirikiano wetu si chaguo bali ni wajibu wa kihistoria kwa ustawi wa watu wetu. Maadui wa Tanzania sio Wakenya na maadui wa Kenya sio Watanzania, Maadui zetu ni ukosefu wa kazi, umaskini na ukosefu wa maendeleo. Hivyo tujitahidi kupambana na maadui hawa ili kujiletea maendeleo na  kuongeza ajira kwa vijana”alisema Mhe. Rais Ruto.

Mhe. Rais Ruto alieleza pia kuwa hatua ya pamoja ya kuwekeza katika miradi mikubwa ni muhimu kwa nchi za Afrika Mashariki ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya ukanda na kuongeza kuwa Afrika Mashariki ina rasilimali za kutosha, lakini kinachohitajika ni maamuzi ya pamoja na uwekezaji wa kimkakati ili kuzitumia kikamilifu rasilimali hizo.

Moja ya miradi mikubwa iliyotajwa ni ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha mafuta katika Mji wa Tanga ambacho kinatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa ukanda mzima, kwani kitahakikisha mafuta ghafi yanachakatwa ndani ya nchi badala ya kusafirishwa nje.

Alisema Uwekezaji katika mradi huo wa Tanga gharama zake ni kubwa ambao unafikia mabilioni ya dola na kubainisha kuwa Kenya imeamua kuunga mkono ujenzi wa kiwanda hicho nchini Tanzania kama ishara ya mshikamano wa kikanda.

Mhe. Rais Ruto alieleza kuwa uchaguzi wa  kuamua kuiunga mkono Tanga unatokana na uwepo wa miundombinu muhimu kama Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambalo litarahisisha usafirishaji na usambazaji wa mafuta na alisisitiza kuwa huo ni mwanzo wa safari mpya ya Afrika Mashariki kuelekea kujitegemea, umoja na ustawi wa pamoja

Alieleza kuwa kupitia mradi huo, mapato yatabaki ndani ya nchi za Afrika Mashariki, hali itakayosaidia kukuza uchumi wa ndani pamoja na kuongeza ajira kwa maelfu ya vijana. “Hii ni hatua inayolenga si tu maendeleo ya sasa, bali pia mustakabali wa kizazi kijacho,” alisisitiza Rais Ruto.

Rais Ruto pia alizungumzia uhusiano wa kindugu na kihistoria kati ya Tanzania na Kenya, akibainisha kuwa mataifa hayo mawili yameunganishwa na historia, utamaduni na mahusiano ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi. Alitoa wito wa kuendeleza urafiki huo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azan Zungu, alimshukuru Mhe. Rais Ruto kwa hotuba yake ambayo alisema imeakisi dhamira ya kweli ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya na ule wa kikanda, akisisitiza nafasi ya mabunge katika kuweka mazingira wezeshi ya kisera kwa ajili ya maendeleo.

Hotuba hiyo imeelezwa kuwa ya kihistoria, ikitoa dira ya ushirikiano mpana zaidi katika nyanja za nishati, biashara na miundombinu, huku ikisisitiza mshikamano kama nguzo kuu ya maendeleo ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Hakuna maoni: