WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amesema usimamizi na uhifadhi wa mazingira hauwezi kufanikiwa kwa kauli au sera pekee, bali kwa vitendo vinavyoonekana katika ngazi zote, ikiwemo shughuli za upandaji na utunzaji wa miti.
Amesema maono na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni makubwa na yanahitaji ubunifu wa hali ya juu katika utekelezaji wake, hususan kwenye mikakati ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Masauni aliyasema hayo Mei 15, 2026 wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa zoezi la upandaji miti lililoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika Juni 5 mwaka huu, ambapo kitaifa yataadhimishwa mkoani Dodoma.
Amesema Dira ya Taifa ya 2050 ina nguzo kuu tatu, huku moja ya nguzo hizo ikiwa ni uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo linapaswa kupewa uzito mkubwa na kila mwananchi.
“Haya tunayoyaona leo kama mafuriko, ukame na hali ya hewa isiyotabirika ni sehemu ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Kama taifa, ni lazima tutoe kipaumbele katika kukabiliana na changamoto hizi ili kulinda maisha na maendeleo ya wananchi,” amesema Masauni.
Aidha, amesema faida ya upandaji miti inaweza isionekane mara moja, lakini miti hiyo ina mchango mkubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hususan katika kulinda mazingira na kuhakikisha uwepo wa rasilimali endelevu kwa miaka mingi ijayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Masauni ameipongeza Wilaya ya Kilosa pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa kuwashirikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kampeni za upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
Mhe. Masauni aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, akiwemo Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Balozi Baraka Luvanda, ambaye alisema zoezi hilo lilianza tangu jana na tayari zaidi ya miti elfu 40 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema wilaya hiyo imejiwekea lengo la kupanda miti milioni 1.5, huku zoezi hilo likiendelea kufanyika kila mwaka kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo.
Amesema Wilaya ya Kilosa imekuwa ikikabiliwa mara kwa mara na changamoto ya mafuriko, hivyo serikali imepanga kujenga mabwawa ya maji katika maeneo ya Mto Mkondoa ili kudhibiti athari hizo. Ameongeza kuwa upandaji wa miti utasaidia kulinda vyanzo vya maji na miundombinu hiyo, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni