Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es salaam-UDART, Waziri Kindamba, amesema Mabasi 99 ya mwendokasi yanatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Mabasi hayo 99 yalitakiwa kuwasili nchini mwezi agosti na kwamba yamechelewa kutokana na mchakato wa manunuzi.
Mwezi Mei mwaka huu, UDART inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 85, na asilimia 15 ni Simon Kisena kupitia Simon Group, ilipokea basi moja kati ya 100 kwa ajili ya majaribio na kumjulisha mzalishaji kutengeneza mengine ambayo tayari yameshakamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, Kindamba amewaambia wanahabari jijini Dar es salaam kuwa kuchelewa kwa mabasi hayo kunatokana na mchakato wa ununuzi serikalini ambao lazima ufuatwe.
Kwa mujibu wa Kindamba basi moja lenye uwezo wa kubeba abiria 150 linanunuliwa kwa shilingi Milioni-500 hivyo kwa mabasi hayo 100 zaidi ya shilingi Bilioni-50 zinatumika kuyanunua.
Kuwasili kwa mabasi hayo kunatajwa kutasaidia kutoa nafuu ya usafiri jijini Dar es salaam kwa njia ya Kimara-Kivukoni, na kwamba yataletwa mengine kwa kuwa udart imesahakamilisha andiko la mradi na kuwasilisha Benki ya NMB ambao wameridhia kuwapa mkopo.
“Ni kwamba maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kutatua kero ya usafiri jijini Dar es Salaam, tunatekeleza kwa vitendo kwa kuhakikisha njia zote sita za Kimara, Mbagala, Tegeta, Ubungo, Gongo la Mboto na nia za kati za kuunga mwendokasi zinakuwa na mabasi ndani ya mwaka huu 2025 ”amesema Kindamba.
Amewaomba wakazi wa jiji la Dar es salaam kuwa wavumilivu wakati wakisubiri kuwasili kwa mabasi mapya 99 yanayotumia gesi akiwa pia na viyoyozi ndani yake.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni