Shilingi milioni 100 zimetolewa na Benki ya CRDB kupitia mbio za CRDB msimu wa sita kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika leo katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema mbio hizo zimeyaunganisha mataifa 27 na kuwakutanisha washiriki zaidi ya elfu 16 ambao kwa kukimbia kwao wameweza kuchangia matibabu ya watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo.
Dkt. Tulia amesema CRDB Benki imeweza kusambaza tabasamu kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuhakikisha watoto zaidi ya 500 wenye magonjwa ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na afya zao kurejea.
Aidha Mhe. Dkt. Tulia aliwashukuru wadau wa Benki ya CRDB kwa kuungana na benki hiyo kukusanya fedha kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, wanawake wenye ujauzito hatarishi na vinajana wanaohitaji kuinuliwa kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji kutoka Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema mbio za CRDB msimu wa sita zinaenda sambamba na kusherehekea miaka 30 ya benki hiyo huku akiainisha kuwa kwa kipindi chote hicho benki hiyo imekuwa ikichukua asilimia 1 ya pato lake na kurudisha katika jamii kupitia michezo, afya, elimu na mambo mengine.
Nsekela amesema misimu sita ya mbio za CRDB imekuwa ikiwawezesha wadau wake wakuu watatu wakiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya CCBRT na Vijana kupitia programu mbalimbali za maendeleo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni