Breaking


Jumatano, 13 Agosti 2025

KATAVI WAMPA HEKO RAIS SAMIA UMEME VIJIJINI


Wananchi wa Kijiji cha Mapili Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kubadili maisha yao kupitia mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini-REA.

Wametoa shukrani hizo wakati wa kampeni maalum ya uhamasishaji wa matumizi ya umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali kote nchini.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kabla ya kupata nishati hii ya umeme mazingira hayakuwa mazuri, usiku hatukuwa na mwanga sasa hivi tunaishi kwa amani na hata baadhi ya shughuli za kimaendeleo zinafanyika hadi muda wa usiku lakini pia tunapata habari kwa kutazama luninga muda wowote tunaotaka pia baadhi ya vijana wamepata ajira kupitia umeme,” alisema Mwalimu Mstaafu, Mkazi wa Kijiji cha Mapili, Amos Katawa.

Naye, Scholastica Kitwewe, Mkazi wa Kijiji cha Mapili alisema umeme umerahisisha maisha ya wanawake kijijini hapo kwani hapo awali walikuwa wakitumia muda mwingi kuandaa mahindi ya unga kwa kutwanga katika kinu lakini sasa mashine za kusaga na kukoboa nafaka zimefunguliwa kijijini hapo jambo ambalo linarahisisha shughuli zao za mapishi ya kila siku na kuwaokolea muda.

Akizungumza kuhusu umeme kijijini hapo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mapili Anthony Mwijuma, aliipongeza REA kwa kutekeleza mradi huo ambao alisema umekuwa ni neema kwa wananchi wake ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kufikiwa na umeme.

Akizungumza hali ya usambazaji umeme mkoani Katavi, Msimamizi wa miradi ya REA Mkoani humo, Gilbert Furia, alisema vijiji vyote vina umeme na kazi inayoendelea sasa ni kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havikufikiwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu aliipongeza REA kwa kukamilisha mradi wa kufikisha umeme vijijini na alisema kuwa amejionea namna ambavyo kazi ya kufikisha umeme vitongojini ikiendelea kutekelezwa kwa kasi. 

Hakuna maoni: