Breaking


Ijumaa, 1 Agosti 2025

MAJINA YA MAWAKALA YAPELEKWE SIKU 7 KABLA YA UCHAGUZI MKUU-INEC



Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi-INEC, imetangaza kuwa mwaka huu mgombea pekee wa nafasi ya ubunge au udiwani atapigiwa kura ya ndio au hapana.

Atakuwa amechaguliwa kihalali kuwa mbunge au diwani ikiwa atapata kura nyingi za ndio kati ya kura zote halali zilizopigwa.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima wakati wa mkutano wa kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kailima, endapo mgombea huyo atashindwa kupata idadi ya kura zinazohitajika, msimamizi wa uchaguzi ataitaarufu tume kuhusu matokeo hayo na tume itapanga siku nyingine ya uteuzi kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuwasilisha orodha ya majina ya mawakala wa uchaguzi siku saba kabla ya siku ya uchaguzi, ambapo kwa uchaguzi huu itakuwa ni tarehe 22, oktoba 2025.

Uchaguzi mkuu wa mwaka huu umepangwa kufanyika Oktoba 29 siku ya Jumatano.

Hakuna maoni: