Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amerejesha rasmi fomu za uteuzi katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma. Alifuatana na Mgombea Mwenza Balozi Emmanuel John Nchimbi.
Baada ya kurejesha fomu hizo, Dkt. Samia aliwashukuru wanachama wa CCM waliomdhamini kwa niaba ya mamilioni ya wanachama wa chama hicho kutoka kila pembe ya nchi.
“Ninawashukuru sana wanachama wa CCM waliowakilisha mamilioni ya wenzetu kutoka kila pembe ya nchi kwa kuniunga mkono katika fomu za udhamini,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, aliwaomba Watanzania kuendeleza mshikamano na mshikikano wa kitaifa wakati taifa likielekea kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi.
“Tunapoelekea kuzindua kampeni za uchaguzi, tuendelee kudumisha umoja huu ili kukihakikishia chama chetu ushindi. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, turejee kuendelea kuwatumikia wananchi kama yalivyo matarajio yao,” aliongeza.
Hatua hiyo imeashiria rasmi mwanzo wa safari ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni