Takriban Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu 700 wa mashirika ya umma nchini wanatarajiwa kushiriki katika kikao kazi maalum, CEO Forum 2025, kitakachofanyika Agosti 23–26 jijini Arusha, kwa lengo la kujadili nafasi ya taasisi hizo katika uchumi wa kisasa na ushindani wa kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Agosti 11, 2025, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Umma ya Kibiashara, Lightness Mauki, amesema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na ubunifu ndani ya taasisi za umma.
Mauki ameeleza kuwa CEO Forum 2025 inalenga kuchochea mabadiliko ya kimfumo ili taasisi za umma ziweze kuongeza mapato yasiyo ya kodi, kuwa washindani wa kweli katika soko la kimataifa, na kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa kisasa unaoongozwa na matokeo.
Mkutano huo utakuwa jukwaa la kujadili changamoto, fursa na mikakati ya mageuzi ya kitaasisi kwa lengo la kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa juu, pato la Taifa la dola trilioni 1, na pato la mtu mmoja mmoja la dola 7,000 kwa mwaka.
Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni: “Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara Katika Mazingira Shindani Kimataifa – Nafasi ya Mashirika ya Umma,” ikilenga kuhimiza taasisi za umma kubadilika kutoka mifumo ya zamani na kuelekea kwenye uendeshaji wa kisasa wa kibiashara na ushirikiano.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni