Breaking


Jumatatu, 25 Agosti 2025

TFS YAONGOZA TUZO YA USIMAMIZI BORA WA FEDHA 2025



Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kung’ara kitaifa baada ya kutwaa Tuzo ya Usimamizi Bora wa Fedha kwa Taasisi zisizo za Kibiashara 2025, katika Mkutano wa wa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Serikali (CEOs Forum 2025) uliofanyika jijini Arusha.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa leo Agosti 24, 2025 na Makamu wa Rais, Dk. Philip Isdor Mpango, 

wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa TFS, Adv. Piensia Christopher Kiure, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi akiwa ameambatana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi-Mhasibu Mkuu wa TFS, CPA[T] Peter Mwakosya aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi.

Katika taarifa yake, Mchechu alisema ushindani ulikuwa mkali kwani ulihusisha taasisi zote za Serikali zisizo za kibiashara ambazo zimefanya vizuri katika usimamizi wa fedha,utawala bora na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali.

“Katika Kundi hili Taasisi 5 ziliibuka kuwa bora:TFS, TIRA, BRELA, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) na NBS, ambapo TFS  iliibuja mshindi wa kwanza,” alisema.

Kwa upande wake, Adv. Piensia Kiure alisema ushindi huo ni matokeo ya nidhamu ya kifedha iliyojengwa tangu kuanzishwa kwa wakala huo mwaka 2011.

“Kwa miaka 14 sasa, TFS imekuwa ikipata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku mapato yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka. Tumeboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha, kuzingatia maelekezo ya Serikali, Wizara na bodi ya ushauri, alisema.

Aliongeza kuwa TFS imejijengea heshima kimataifa kupitia ushirikiano na nchi kama Brazili na Urusi kubadilishana uzoefu wa sekta ya misitu, hatua inayoiweka taasisi hiyo kwenye viwango vya ubora wa kimataifa.

“Tuzo hii ni chachu kwetu kuendelea kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu za serikali katika shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu. Ushirikiano wetu na wananchi umeendelea kuimarika, na tunatarajia mafanikio makubwa zaidi,” alisisitiza.

Kufuatia ushindi wa TFS, Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea Tuzo kutokana na kuisimamia vizuri na kutoa mchango mkubwa  kwa Wakala. Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Pindi Hazara Chana.

Mkutano huo wa siku tatu umehudhuriwa na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za serikali, ukiwa na ajenda kuu ya kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika sekta ya umma.

Hakuna maoni: