Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetangaza kampeni mpya ya usafi na uhifadhi wa mazingira, NEMC USAFI KAMPENI 2025, likilenga kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kudhibiti ongezeko la taka ngumu, hususan kwenye maeneo ya mijini. Kwa mujibu wa NEMC, nchi imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na taka ngumu zikiwemo plastiki, ambazo zimekuwa zikitishia afya za wananchi na kuathiri mifumo ya ikolojia. Takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania huzalisha takribani tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka ngumu kila mwaka, sawa na kilo 0.66 hadi 0.95 kwa kila mtu kwa siku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria, Jamal Baruti, alisema jukumu la kulinda mazingira si la serikali pekee bali ni wajibu wa kila Mtanzania. Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano wa pamoja, jamii inaweza kubadilisha mwenendo wa sasa na kuhakikisha hifadhi endelevu ya mazingira kwa vizazi vijavyo.
Aidha, Baruti aliongeza kuwa suala la hifadhi ya mazingira limepewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga Tanzania yenye jamii inayotunza mazingira. Kwa upande wake, Afisa Mazingira Boniface Kiaruzi alisema taka ni fursa na kupitia kampeni hii wananchi watapata elimu kuhusu utunzaji wa mazingira, urejelezaji wa taka na fursa za kiuchumi zitokanazo na usafi wa mazingira.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni