Katika kilele cha heshima kwa michezo ya riadha duniani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mwanariadha wa kimataifa Alphonce Simbu kwa kutwaa Medali ya Dhahabu katika mashindano ya mbio ndefu yaliyofanyika mjini Tokyo.
Kwa muda wa saa 2:09:48, Simbu aliibuka kinara katika mbio hizo, akiiweka Tanzania kwenye ramani ya michezo ya kimataifa na kuandika historia mpya ya taifa.
Rais Samia amesema kuwa ushindi huo ni ishara ya nidhamu, bidii na kujituma kwa kiwango cha juu ambacho kimekuwa alama ya mafanikio ya mwanariadha huyo. Pia amekumbusha ushindi wa Simbu aliposhika nafasi ya pili katika Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni mwendelezo wa safari ya kipekee ya mwanariadha huyo katika michezo ya riadha.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Simbu amekuwa mfano bora wa kuigwa, si tu kwa wanariadha na wanamichezo wenzake, bali pia kwa Watanzania wote, akionesha thamani ya nidhamu na kujituma katika kufanikisha malengo.
Rais Samia amemuhimiza Simbu kuendelea kupeperusha vyema bendera ya taifa na kuliheshimisha taifa la Tanzania katika majukwaa ya kimataifa. Ushindi huu unazidi kuthibitisha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji vya michezo vinavyoweza kushindana na kushinda duniani. 🇹🇿



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni