Breaking


Jumanne, 16 Septemba 2025

TANZANIA NA JAPANI WAZINDUA KAMATI YA PAMOJA YA BIASHARA YA KABONI

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Cyprian Luhemeja, leo amezindua Kamati ya Pamoja kati ya Tanzania na Japani kuhusu Biashara ya Kaboni. 

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira na maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa kamati hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japani katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendeleza miradi yenye tija kwa taifa. 

Ameongeza kuwa kamati hiyo itarahisisha uratibu na ushauri wa kitaalamu, sambamba na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta za nishati safi, kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Japani nchini Tanzania, Mhe. Ueda Shoichi, amesema kuwa ushirikiano huo ni kielelezo cha dhamira ya Japani kushirikiana na Tanzania katika biashara ya kaboni, teknolojia, uwekezaji na maendeleo endelevu, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Hakuna maoni: