Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata masoko ya bidhaa zao.
Akizungumza na wajasiriamali wadogo katika ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil uliopo wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaunda utaratibu maalum wa kuwatafutia masoko wajasiriamali kwa kushirikiana na wawekezaji katika mahoteli makubwa nchini.
Ameeleza kuwa Serikali itakaa na wawekezaji hao ili kuhakikisha wajasiriamali wa ndani wanapata fursa ya kuuza bidhaa zao katika hoteli hizo, hatua itakayoongeza kipato chao na kukuza uchumi wa wananchi.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta soko la uhakika la bidhaa za mwani ndani na nje ya nchi, ili kuwawezesha wakulima wa zao hilo kunufaika zaidi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu 2025.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni