Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa mfano bora wa mafanikio katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF, hatua inayoendana na juhudi za serikali kupunguza umasikini uliokithiri na kuboresha maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Akizungumza katika kikao kazi cha mwaka kuhusu utekelezaji wa TASAF Awamu ya Tatu, Sehemu ya Pili, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Shangwe Twamala, amewataka waratibu wa mpango huo kuhakikisha vikundi vinavyonufaika vinasimamiwa kwa ukaribu na kwa ufanisi.
Twamala amehimiza wanufaika wa mpango huo waendelee kupewa elimu ya ujasiriamali, kusaidiwa kwa mitaji na kupatiwa fursa kupitia mikopo ya asilimia 10 kutoka mapato ya Halmashauri, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kuepuka hali ya umasikini.
Kwa upande wake, Mhandisi Abel Bimbiga kutoka Makao Makuu ya TASAF, ameupongeza mkoa wa Pwani kwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mafanikio katika utekelezaji wa mpango huo.
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema mkoa huo ulikuwa miongoni mwa maeneo ya mwanzo kufanya majaribio ya awali ya mpango huo, na hadi sasa umetekeleza miradi mingi yenye tija kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu, huduma za kijamii na kuinua hali za maisha za wanufaika.
Mpango wa TASAF III Awamu ya Pili unalenga kuwasaidia wananchi walio kwenye mazingira magumu kwa njia ya Ruzuku, ajira za muda, pamoja na uwezeshaji kiuchumi kupitia vikundi vya kuweka na kukopa.
Mwamvua Mwinyi-Pwani





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni