Katika maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yanayoendelea katika Viwanja vya Uhindini mkoani Mbeya, Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO limeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi na vijana wanaotembelea banda lake.Kupitia wataalamu wake, TANESCO limekuwa likitoa mafunzo ya vitendo juu ya namna ya kutumia majiko bora ya kisasa yanayotumia umeme kidogo, salama kwa mtumiaji, na rafiki kwa mazingira.
Akitembelea banda la TANESCO tarehe 9 Oktoba 2025, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Mary Mongela Maganga, alipongeza juhudi hizo na kusisitiza kuwa elimu ya matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa, hususan katika kulinda afya za wananchi na mazingira.
Bi. Mary alisema amevutiwa na teknolojia ya majiko ya kisasa yanayotumia umeme kwa ufanisi mkubwa, akiwataka vijana kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza na kutumia teknolojia hizo katika maisha ya kila siku pamoja na shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake, TANESCO imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wengi zaidi nchini kote, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni