Breaking


Jumanne, 7 Oktoba 2025

WAKULIMA WA MWANI KUNUFAIKA NA SOKO HURU WILAYANI MAFIA

 

Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani, imesisitiza ushindani huru katika soko la mwani ili kumnufaisha mkulima, kuinua pato pamoja na kukuza uchumi wa wilaya hiyo .

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa fedha 2024/2025, mavuno ya mwani yalifikia tani 600 zenye thamani ya sh.milioni 420, kwa bei ya wastani ya Sh.700 kwa kilo.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, anasema serikali inaruhusu ushindani wazi wa wanunuzi wa mwani kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo, bila kuwepo kwa ukiritimba , ama mnunuzi mmoja au kampuni.

Mangosongo ameyasema hayo Oktoba 6, 2025, katika kikao kilichowakutanisha wadau wa kilimo cha mwani wilayani humo, kilicholenga kujadili na kutafuta suluhisho kwa baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima hao ikiwemo uwepo wa mnunuzi mmoja mkubwa, kampuni ya Mwani Mariculture, anayehodhi soko kwa sasa.

Ameeleza Mafia inaenda na azimio la kufungua milango kwa wanunuzi wengine kuingia sokoni, wanataka taratibu zifuatwe na kila kitu kinachowahusu wakulima kipitie halmashauri ili Idara ya Kilimo iwe na taarifa sahihi. 

Aidha, amebainisha kuwa lengo ni kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja, huku bei ya mwani ikitarajiwa kupanda kutoka Sh.800 hadi kufikia Sh.1,000 kwa kilo.

Vilevile Mkuu huyo wa wilaya ameagiza wataalamu wa kilimo, kupata takwimu sahihi kuhusu wakulima waliopo na hali halisi ya zao hilo ili kuwezesha kuweka mikakati ya kiutekelezaji inayoendana na uhalisia wa kilimo cha mwani kisiwani humo.

Rabihu Hemedi, mkulima wa mwani kutoka kijiji cha Banja, ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa vitendea kazi na ujuzi wa kisasa wa kilimo hicho.

Anasisitiza ,elimu kwa wakulima ni muhimu ili kuongeza thamani ya zao hilo, kukuza soko, na kuwezesha uanzishwaji wa ushirika wa wakulima.

Kwa upande wake, Nasri Basha, mkulima kutoka Kiegeani, ameishukuru Serikali ya Wilaya kwa hatua ya kufungua soko na kuomba iendelee kupeleka wataalamu kwa wakulima ili waweze kujifunza mbinu za kilimo cha kisasa cha mwani na kusaidia mchakato wa kuanzisha ushirika rasmi.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya, Alfahad Mohamed, ameeleza licha ya kuuza mwani ghafi, wanaendelea kuhamasisha uongezaji wa thamani ili wakulima watengeneze bidhaa mbalimbali kama sabuni, mafuta, na virutubisho kutokana na mwani. 




Mwamvua Mwinyi-Mafia

Hakuna maoni: