Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Klabu ya Young Africans kwa ushindi wa bao 1–0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Amesema kuwa ushindi huo umeipa nchi heshima kubwa na kuandika historia mpya katika sekta ya michezo, huku Young Africans ikionyesha kiwango cha juu cha ubunifu, nidhamu na ukomavu wa mchezo uliowezesha kupata matokeo mazuri.
Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo kuboresha miundombinu na mazingira ya mchezo, hatua itakayoongeza ushindani wa timu za ndani na kuzisaidia kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Kimataifa.
Aidha, Mhe. Rais amewashukuru mashabiki na wananchi wote waliojitokeza kuisapoti Young Africans SC, akisema kuwa umoja, hamasa na mshikamano waliouonyesha umeufanya Uwanja wa New Amaan Complex kuwa sehemu ya historia muhimu katika safari ya kuendeleza michezo nchini.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni