Katika kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, Serikali ya China kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania imetoa vishkwambi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vitakavyotumika kusajili walipakodi moja kwa moja kutoka kwenye maeneo yao ya biashara, hatua inayolenga kupanua wigo wa walipakodi na kuongeza Mapato ya Serikali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika Novemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam kati ya Balozi wa China, Mhe. Chen Mingjian na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda, CG Mwenda amesema msaada huo utaongeza ufanisi wa TRA katika kuwafikia wananchi na kurahisisha usajili wa walipakodi wapya.
Amesisitiza kuwa kadri idadi ya walipakodi inavyoongezeka, mzigo wa kodi unapungua kwa mtu mmoja mmoja na mapato ya Taifa yanakuwa imara zaidi, hivyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujisajili watakapofikiwa.
Kwa upande wake, Balozi Mhe. Chen Mingjian amesema msaada huo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya China na Tanzania, akiongeza kuwa wapo wawekezaji wengi wa China wanaonufaika na huduma za TRA, hivyo ni muhimu kuendelea kuunga mkono taasisi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Uchumi wa Tanzania.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni