Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Wakala wa Usafirishaji wa Blueberry Travels wametangaza mpango maalum wa kurahisisha safari za mashabiki watakaosafiri kwenda Morocco kuisapoti Taifa Stars kwenye michuano ya AFCON 2025, inayotarajiwa kuanza Desemba 21, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 12, 2025, katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Michezo kutoka BMT, Benson Chacha, amesema mpango huo umeanzishwa kufuatia maombi mengi kutoka kwa mashabiki waliotaka kujua utaratibu wa safari za pamoja.
“Sisi kama Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na TFF tumekuwa tukipokea barua na simu nyingi kutoka kwa mashabiki wakitaka kujua utaratibu wa safari. Kupitia mchakato tuliofanya, tumepata kampuni ya Blueberry Travels ambayo itarahisisha safari za mashabiki wengi kwenda Morocco kuishangilia timu ya Taifa,” amesema Chacha.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema kuwa TFF imeona umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha mashabiki wengi zaidi kwenda kuipa nguvu Timu ya Taifa wakati wa michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Blueberry Travels yaweka wazi gharama za vifurushi
Ofisa Masoko wa Blueberry Travels, Kelvin Charles, ameshukuru BMT na TFF kwa kuiamini kampuni hiyo kuratibu safari hizo. Amesema wameandaa vifurushi rafiki kulingana na vipato vya Watanzania, ambavyo vinajumuisha nauli ya kwenda na kurudi, malazi pamoja na usafiri wa ndani nchini Morocco.
Ameeleza kuwa vifurushi hivyo vimeandaliwa kwa kuzingatia ratiba ya mechi za Taifa Stars, huku mashabiki wakipewa uhuru wa kuchagua idadi ya michezo wanayotaka kushuhudia.
Vifurushi ni pamoja na:
Tanzania vs Nigeria (21 Desemba 2025):
Mtu mmoja: USD 2,53
Wawili: USD 2,320 kwa kila mmoja
Tanzania vs Uganda (27 Desemba 2025):
Mtu mmoja: USD 2,970
Wawili: USD 2,700 kwa kila mmoja
Tanzania vs Tunisia (30 Desemba 2025):
Mtu mmoja: USD 3,000
Wawili: USD 2,780 kwa kila mmoja
Kwa mashabiki wanaotaka kushuhudia michezo yote ya Taifa Stars, vifurushi ni:
Mtu mmoja: USD 5,250
Wawili: USD 4,400 kwa kila mmoja
Charles amesema vifurushi hivyo vimetengenezwa kwa kuzingatia usalama, urahisi wa safari na utoaji wa huduma bora kwa mashabiki.
Mpango huo kwa ujumla unalenga kuongeza hamasa na sapoti kwa Taifa Stars, ili kuwatia moyo wachezaji katika safari yao ya kuiwakilisha Tanzania kwenye AFCON 2025.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni