Breaking

Jumatano, 3 Desemba 2025

TCAA YAMEWEZESHA MAFANIKIO YA REKODI YA DUNIA NDANI YA HIFADHI YA TARANGIRE

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeratibu na kusimamia kwa mafanikio safari ya kihistoria ya puto la hewa moto (hot air balloon) iliyoifanya Tanzania kuorodheshwa rasmi kama nchi ya 123 katika jaribio la rekodi ya dunia la kurusha balloon na rubani akiwa pekee yake, lililoendeshwa na Dkt. Rubani Allie Dunnington.

Safari hiyo maalum imefanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ikiwa ni mara ya kwanza kwa safari ya aina hii kufanyika na mtu mmoja ndani ya eneo la hifadhi. Uamuzi huu wa kipekee ulifikiwa na TCAA baada ya kufanya tathmini ya kina ya kiusalama, utaratibu wa kiufundi na uhalali wa operesheni ndani ya eneo hilo nyeti.

Kwa mujibu wa TCAA, safari hiyo imefuata kikamilifu kanuni, taratibu na viwango vya usalama vya kitaifa na kimataifa. TCAA imeshirikiana kwa karibu na wadau wa uhifadhi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha zoezi linafanyika kwa usalama, ufanisi na kulinda uadilifu wa mazingira ya hifadhi.

Dkt. Rubani Allie Dunnington, ambaye anaendelea na safari yake ya kuzunguka dunia kwa kutumia puto, ameipongeza TCAA kwa ushirikiano, weledi na uratibu uliomwezesha kutimiza hatua hii muhimu ya kihistoria. Alieleza kuwa kuruka juu ya Tarangire kumeongeza thamani ya jaribio lake na kutoa taswira adimu ya uzuri wa Tanzania kutoka angani.

Mafanikio haya yanaendelea kuiongezea Tanzania hadhi katika ramani ya kimataifa kama taifa lenye mifumo madhubuti ya udhibiti wa anga, usimamizi bora wa usalama, na utayari wa kushirikiana katika shughuli za kimataifa zinazochochea maendeleo ya sekta ya anga na utalii.

Hakuna maoni: