Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) imesaini hati ya Makubaliano na Kampuni ya Africa Global Logistics ( AGL) Tanzania Ltd yenye Makao Makuu yake Nchini Ufaransa ambayo ni kampuni tanzu ya MSC, kwa ajili ya usanifu, Ujenzi na uendeshaji wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo.
Hati hii ya makubaliano ( MoU) imesainiwa tarehe 6 Disemba,2025 Makao Makuu ya TPA Jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Plasduce Mbossa na Rais wa AGL Philippe Labonne.
Mbossa amesema, kusainiwa kwa hati ya Makubaliano ni ishara ya utayari wa kuanza kwa mradi wa Bandari mpya ya Bagamoyo ambapo kwa kuanzia AGL itaanza usanifu na Ujenzi wa gati tatu mpya za Kisasa kati ya 28 zinazotatajiwa kujengwa katika Bandari hiyo pamoja na gati mbili mpya za Kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunategemea kuanza Ujenzi wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo mapema mwezi Januari na pia tunawakaribisha Wawekezaji wengine wa ndani na wa nje katika Mradi huo ambapo lengo ni kuleta mapinduzi makubwa katika Shughuli za Kibandari Nchini” Amesema Bw. Mbossa.
Kwa upande wake Rais wa AGL Bw. Philippe Labonne anasema wameamua kuingia makubaliano na TPA na kuwekeza Tanzania kutokana na kuwa nchi yenye Amani, Usalama na mazingira bora na tulivu ya uwekezaji iliyosehemu sahihi kijiografia kwa Sekta ya Uchukuzi na kuwa lango la Biashara Kitaifa na kimataifa.
“ Ninaamini Tanzania ni nchi inayokuwa kwa kasi kimaendeleo ikiwa na mtaji Mkubwa wa watu wakatimu na mtazamo Chanya na pia ni lango la kuingilia nchi nyingi barani Afrika na kuyafikia masoko ya kimataifa, Naamini ushirikiano huu utafungua mambo mengi ikiwemo kutengeneza Ajira ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya Mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla” Amesema Bw. Labonne.
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kwa gati mpya tatu utajengwa kwa miezi 36 ( miaka mitatu) na Kampuni ya AGL imepata nafasi hii ya kushirikiana na TPA katika Ujenzi huo kutokana na uzoefu wao kama kampuni kubwa ya huduma za usafirishaji na logistiki, inayotoa huduma kamili za usafirishaji, usimamizi wa mizigo, usafirishaji wa kimataifa na huduma za forodha, ikihudumia sekta mbalimbali kama uchimbaji, mafuta, chakula, na misaada ya kibinadamu, ikiwa sehemu ya kundi la kimataifa la AGL (zamani Bolloré T&L) na sasa wakiwa chini ya MSC.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni