Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua rasmi matumizi ya mita janja mpya za umeme, hatua inayoashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma na uboreshaji wa mifumo ya nishati nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amelielekeza TANESCO kuhakikisha mita janja zinasambazwa katika mikoa yote nchini ili kuongeza ufanisi, kurahisisha huduma kwa wateja na kuendana na maendeleo ya kiteknolojia.
Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa mifumo ya mita hizo inapaswa kuboreshwa kila mwaka ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya watumiaji, sambamba na kuharakisha huduma kwa wateja wapya wanaohitaji kuwekewa mita.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mita janja zina faida nyingi ikiwemo uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu na kutoa suluhisho endapo mteja atanunua umeme kwa bahati mbaya au kukosea taarifa.
“Mita hizi zinabeba taarifa zote muhimu kuhusu mwenendo wa matumizi ya umeme, hivyo zitapunguza mawasiliano ya mara kwa mara kati ya shirika na wateja. Pia zina mifumo madhubuti ya usalama na kulinda uthibiti wa mapato,” amesema Twange.
Ameongeza kuwa moja ya faida kubwa kwa wateja ni kwamba umeme unaingia moja kwa moja kwenye mita pindi unaponunuliwa, bila kungoja token au kutumia remote, hali inayomuepusha mteja na usumbufu wa kukosa betri au kuchelewa kwa aliyekuwa akimiliki kifaa hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kati ya wateja zaidi ya milioni 5.5 wa TANESCO, zaidi ya milioni 1.5 wanapatikana Dar es Salaam, hivyo mkoa huo unatarajiwa kuwa kitovu cha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mfumo huo.
Uzinduzi huu unatajwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya kidijitali ya sekta ya nishati, inayolenga kuongeza uwazi, kuimarisha ufanisi na kupunguza changamoto za muda mrefu katika usambazaji na udhibiti wa umeme nchini.









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni