Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limemfungia Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o, kujihusisha na shughuli za soka kwa mechi nne, kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Mbali na kifungo hicho, CAF pia imemtoza Eto’o faini ya dola 20,000 za Marekani, ikieleza kuwa alikiuka misingi ya uungwana na maadili ya michezo. Tukio hilo linadaiwa kutokea wakati wa mchezo wa robo fainali kati ya Cameroon na Morocco uliofanyika Januari 9.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Eto’o alionekana kuonesha hasira kali kufuatia baadhi ya maamuzi ya mwamuzi wakati wa mchezo huo, hali iliyozua sintofahamu uwanjani. Cameroon ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-0 dhidi ya Morocco, ambao walikuwa wenyeji wa mashindano hayo.
Rais wa CAF, Patrice Motsepe, ambaye alikuwepo uwanjani wakati wa mchezo huo, anaripotiwa kushuhudia moja kwa moja tabia ya kutoridhika iliyooneshwa na Eto’o. Siku chache baadaye, Januari 12, CAF ilitangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu matukio ya vurugu na mienendo isiyokubalika miongoni mwa wachezaji na maofisa wa timu mbalimbali.
Hata hivyo, FECAFOOT imepinga vikali uamuzi huo wa CAF, ikieleza kuwa mchakato mzima unaacha maswali makubwa kuhusu haki na usikilizwaji wa kesi kwa uwazi. Kupitia taarifa yake ya Jumatano, shirikisho hilo limethibitisha kumuunga mkono Rais wake na kudokeza kuwa Eto’o atakata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.
Tangu achaguliwe kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon mwaka 2021, taswira ya Samuel Eto’o kama gwiji wa soka barani Afrika imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya mara kwa mara. Amekuwa akikabiliwa na lawama kuhusu utendaji, uongozi na madai ya ukiukwaji wa taratibu ndani ya FECAFOOT.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 44 ameendelea kukanusha tuhuma hizo, akisisitiza kuwa amepata mafanikio makubwa katika juhudi za kuimarisha na kuendeleza soka la Cameroon tangu alipoingia madarakani.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni