Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Jengo jipya la kisasa la Ofisi za Wizara ya Fedha lililopo Mji wa Serikali-Mtumba, mkoani Dodoma, litawawezesha watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi katika mazingira bora na kuwahudumia wananchi na wadau wake wengine kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Balozi Omar, amesema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo hilo akiambatana na Naibu Mawaziri wake wawili, Mhe. Larent Luswetula, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde, na Menejimenti ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha jengo hilo kujengwa na kukamilika.
Mhe. Balozi Omar, aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kulitunza Jengo hilo na kuhakikisha kuwa mifumo yake ya ulinzi na usalama inasimamiwa ipasavyo.
Wakizungumza katika ziara hiyo, Naibu Mawaziri, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) na Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), walisema kuwa Jengo hilo ni la kisasa na limejengwa kwa viwango vya hali ya juu.
Akitoa taarifa wa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo hilo kutoka Wizara ya Fedha, Mhandisi Japhet Mkwamira, alisema kuwa ujenzi wa Jengo lenye ghorofa 11 ambalo ni Jengo refu kuliko majengo yote ya Serikali yaliyopo Mji wa Serikali-Mtumba kwa sasa, limekamilika kwa asilimia 98.
Jengo hilo la Wizara ya Fedha, linajengwa na Mkandarasi Mkuu Kampuni ya Estim Construcion Co. Ltd, na Mshauri Elekezi wa mradi, ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) likishirikiana na IPA Architects Ltd katika Usanifu na Usimamizi wa ujenzi.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni