Breaking


Jumamosi, 24 Januari 2026

MUHIMBILI YAWASOGEZEA WANANCHI ZANZIBAR HUDUMA ZA KIBINGWA BOBEZI KUPITIA KAMBI KUBWA YA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MAGONJWA MBALIMBALI

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kufanya kambi maalum ya siku nne ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa Zanzibar, itakayofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 6 Februari 2026 katika viwanja vya Amani Complex, kisiwani Unguja.

Kambi hiyo itahusisha madaktari bingwa bobezi kutoka Muhimbili kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wa Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa, hususan katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani, amesema magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuongezeka na kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma, akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa afya mapema ili kuyagundua na kuyadhibiti katika hatua za awali.

Kwa upande wake,Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo Dkt. Robert Moshiro, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema kambi hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Muhimbili na Zanzibar, sambamba na kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kwa wataalamu wa afya. Ameongeza kuwa wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo makubwa watapatiwa rufaa kwa matibabu zaidi katika vituo husika.

Naye Meneja wa Vodacom Foundation Tanzania, Bi. Sandra Oswald, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya Zanzibar. Ameeleza kuwa kambi kama hizo tayari zimefanyika katika mikoa tisa ya Tanzania Bara na kuwafikia zaidi ya wananchi elfu kumi.

Katika kambi hiyo, wananchi watapata huduma za uchunguzi, matibabu pamoja na elimu ya afya kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya kinamama na afya ya uzazi, saratani, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, figo, meno, ngozi, macho, masikio, pua na koo, pamoja na huduma za dharura.

Huduma zitatolewa kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kwa siku zote nne, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi wote bila kikwazo cha umbali.

Hakuna maoni: