Breaking


Jumamosi, 24 Januari 2026

NMB YAZINDUA MFUMO MPYA WA MALIPO YA KISASA KUPITIA PETE, BANGILI NA STIKA NCHINI TANZANIA



Benki ya NMB imeandika historia mpya katika sekta ya huduma za kifedha nchini baada ya kuzindua rasmi mfumo wa kisasa wa malipo kwa kutumia vifaa vinavyovaliwa, maarufu kama NMB Tap Wearables, ikiwa ni mara ya kwanza teknolojia hiyo kuanzishwa Tanzania.


Mfumo huo unamwezesha mteja kufanya malipo kwa kugusa tu kifaa chake cha pete, bangili au stika maalum, ambavyo vinaunganishwa moja kwa moja na akaunti ya benki ya NMB, bila kutumia kadi au fedha taslimu. Hatua hiyo inalenga kurahisisha miamala ya kifedha na kuongeza usalama pamoja na ufanisi wa malipo ya kila siku.


Uzinduzi wa huduma hiyo umefanywa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, akiambatana na Innocent Yonazi, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa benki hiyo.


Kwa upande wa washirika wa teknolojia ya malipo, kampuni ya Mastercard imewakilishwa na Moses Alphonce, Meneja Biashara wa Mastercard Tanzania.


Akizungumza katika uzinduzi huo, uongozi wa NMB umeeleza kuwa huduma ya NMB Tap Wearables ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo wa kuendelea kuongoza safari ya ubunifu katika huduma za kifedha, kwa kuzingatia mahitaji ya wateja na mabadiliko ya teknolojia ya kimataifa.


Kupitia huduma hii, NMB inalenga kuwapa wateja wake uzoefu wa kisasa zaidi wa kifedha, unaoendana na kasi ya maisha ya sasa, huku ikiimarisha nafasi yake kama kinara wa mageuzi ya huduma za kifedha nchini Tanzania.


Hakuna maoni: