Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ametangaza rasmi kuwa Kitita cha Huduma Muhimu cha Bima ya Afya kwa Wote awamu ya kwanza, kwa kundi litakalogharamiwa na Serikali, kitaanza kutumika Januari 26, 2026.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyotoa ndani ya siku 100 za uongozi wake, ya kuhakikisha wananchi wote, hususan wasiokuwa na uwezo, wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya gharama.
Katika awamu hiyo, wananchi 1,457,602 sawa na kaya 276,004 zisizo na uwezo zitasajiliwa na kugharamiwa kikamilifu na Serikali.
Waziri Mchengerwa ametoa tangazo hilo Januari 23,2026, Mkoani Dodoma wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali.
Amesema utekelezaji wa mpango huo unatokana na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Sura ya 161, kifungu cha 13, ambacho kimeanzisha Kitita cha Mafao ya Huduma Muhimu, na kwa mujibu wa Kanuni ya 31(4) ya Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote T.S Na. 809 za Mwaka 2024, Waziri wa Afya ana mamlaka ya kutangaza rasmi kwa Umma kitita cha huduma zitakazotolewa na Skimu za Bima ya Afya nchini.
“Kwa kuzingatia Sheria na Kanuni tajwa hapo juu, natangaza kwa Umma kuwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote itahusisha wananchi wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao watagharamiwa na Serikali,” amesema Waziri Mchengerwa.
Amefafanua kuwa gharama ya Kitita cha Huduma Muhimu ni Shilingi 150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, ikijumuisha mwanachama mchangiaji, mwenza wa mwanachama na wategemezi wanne, ambao ni mzazi wa mwanachama au mzazi wa mwenza wake, mtoto wa kuzaa, kuasili au wa kambo aliye chini ya miaka 21, au ndugu wa damu aliye chini ya umri huo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, huduma zitakazotolewa chini ya kitita hicho zitazingatia utaratibu wa Rufaa katika vituo vya kutolea huduma za afya vitakavyoingia mkataba na Skimu za Bima ya Afya, huku orodha ya huduma hizo ikiwa imeambatishwa katika kiambatisho maalum.
“Hivyo, natangaza rasmi kuwa Kitita cha Huduma Muhimu cha Bima ya Afya kwa Wote awamu ya kwanza kitaanza kutumika tarehe 26 Januari, 2026 kwa kundi litakalogharamiwa na Serikali,” amesisitiza.
Kadhalika, Waziri Mchengerwa amewaagiza viongozi na wataalamu wanaohusika kuendelea na zoezi la utambuzi wa kaya zisizo na uwezo, kwa kushirikiana na mamlaka husika, ili kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa na kunufaika na mpango huo muhimu wa kitaifa.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni