Serikali imewekeza zaidi ya shilingi Trilioni-10 katika miradi 22 ya ujenzi, upanuzi na maboresho ya bandari kote nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini na kukuza uchumi wa taifa.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay, iliyopo Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma.
Akizungumza na viongozi wa Serikali, wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania-TPA na wananchi wa eneo hilo, Waziri Mbarawa, amesema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay kwa shilingi Bilioni-81 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa chini ya Wizara ya Uchukuzi, hususani katika Maziwa Makuu kwa lengo la kuimarisha biashara ya kikanda na usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dokta Baraka Mdima, amesema mradi wa Bandari ya Mbamba Bay, umefikia Asilimia 47 na unaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, usalama na utunzaji wa mazingira.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni