Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) imetoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa serikali wa kusitisha kwa muda huduma za intaneti nchini humo wakati wa uchaguzi mkuu, ikieleza kuwa hatua hiyo imelenga kulinda amani, usalama wa taifa na uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.
Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, UCC ilisema kuzimwa kwa intaneti kulilenga kuzuia usambazaji wa taarifa potofu, vitendo vya wizi wa kura pamoja na shinikizo la mtandaoni linaloweza kuchochea ghasia au vurugu wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, tume hiyo ilisisitiza kuwa si taasisi zote zilizoathiriwa na hatua hiyo, ikibainisha kuwa huduma za intaneti ziliendelea kupatikana kwa taasisi za msingi ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu muhimu ya kitaifa haukwamishwi.
“Taasisi zinazotegemea intaneti lakini zisizo za msingi zitaendelea kukosa huduma ya intaneti katika kipindi hiki cha uchaguzi,” ilieleza sehemu ya taarifa ya UCC.
UCC pia imewahimiza wafanyabiashara na watoa huduma wanaoamini kuwa shughuli zao ni za msingi lakini wameathiriwa na zuio hilo, kuwasilisha maombi rasmi kwa maandishi ili yafanyiwe tathmini upya. Kwa mujibu wa tume hiyo, maombi hayo yatachunguzwa na kamati ya usalama kabla ya kuamuliwa iwapo huduma husika zitaruhusiwa kuendelea kutumia intaneti.
Licha ya maelezo hayo, kuzimwa kwa intaneti wakati wa chaguzi si jambo jipya nchini Uganda. Katika uchaguzi wa mwaka 2021, intaneti ilizimwa kwa takribani wiki moja, hali iliyodaiwa kuathiri upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wapiga kura na kuripotiwa kuhusishwa na vifo vya watu kadhaa.
Safari hii, hatua hiyo imekuja wakati ambapo Ofisi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini Uganda imesimamisha vibali vya angalau mashirika sita na kufunga kwa muda akaunti zao za benki, jambo lililozua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kushirikiana unaolindwa na Katiba ya Uganda na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.
Aidha, mapema mwezi huu, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilitoa tahadhari kuhusu vikwazo vya taarifa kabla ya uchaguzi nchini humo, ikieleza wasiwasi wake juu ya vitendo vinavyodaiwa kuwa ni unyanyasaji, vitisho, kukamatwa kiholela na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari.
Hatua ya serikali ya Uganda ya kuminya upatikanaji wa intaneti inaendelea kuzua mjadala mkali kati ya hoja za usalama wa taifa na hitaji la kulinda haki za msingi za raia katika kipindi nyeti cha uchaguzi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni