Breaking


Jumapili, 25 Januari 2026

UWEKEZAJI KATIKA MICHEZO CHACHU YA MAENDELEO NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema maendeleo makubwa ya michezo nchini yametokana na juhudi na maono ya viongozi wakuu wa nchi, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, walioweka michezo kuwa kipaumbele cha kitaifa.

 Masauni ameyasema hayo tarehe 24 Januari, 2026, wakati wa hafla ya kufunga Mashindano ya Mpira wa Pete ya Kombe la Muungano Zanzibar, ambapo timu ya KVZ imeibuka bingwa baada ya kushinda michezo yote kumi.

Amesema kupitia mpango wa Goli la Mama, kumekuwa na ongezeko la bajeti ya michezo, ujenzi wa viwanja vipya pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya wanamichezo, hali iliyochangia mafanikio ya Timu ya Taifa ya mpira wa miguu, Taifa Stars, kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON nchini Morocco, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya ushiriki wa Tanzania.

Aidha, Waziri Masauni amesema ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya michezo umewezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya kimataifa ikiwemo michuano ya CHAN iliyoshirikisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, jambo linaloonesha kupanda kwa hadhi ya nchi kisoka barani Afrika na duniani.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia wizara husika na taasisi za michezo zikiwemo ZFF, TFF, CHANEZA na CHANETA.

Masauni amewapongeza viongozi wa taasisi hizo kwa usimamizi mzuri wa michezo na mchango wao katika kuimarisha Muungano kupitia sekta ya michezo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHANEZA, Bi. Nasra Juma, ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushiriki na kudhamini mashindano hayo, akisema yamekuwa na ushindani mkubwa na yameendelea kutoa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Mashindano ya Kombe la Muungano Zanzibar yalishirikisha jumla ya timu kumi na moja, tano kutoka Zanzibar na sita kutoka Tanzania Bara.

Hakuna maoni: