Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufuatilia na kuimarisha utekelezaji wa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi za magonjwa ya moyo kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kusogeza huduma maalum za afya karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
Katika ziara hiyo, Dkt. Samizi amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, ambapo wamejadili kwa kina uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya afya mkoani Arusha, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na ongezeko la wataalamu wa afya.
Dkt. Samizi amesema uwekezaji huo umeongeza uwezo wa Mkoa wa Arusha kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na wageni, huku akibainisha kuwa maboresho hayo yataendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya wakati wa mashindano makubwa ya AFCON 2027, jambo litakaloiwezesha Arusha kukidhi mahitaji ya kiafya kwa viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, amesema Mkoa umeanza maandalizi ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kuimarisha uhamasishaji na maandalizi katika ngazi za Wilaya, Kata na Mitaa, akisisitiza kuwa mpango huo utaongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia, huku viongozi hao wakiwapongeza watumishi wa sekta ya afya kwa kazi kubwa na ya kujitolea wanayoendelea kufanya.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni