Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo, amelielekeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuimarisha utafiti na ubunifu katika sekta ya ujenzi ili kubuni mbinu na teknolojia zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata nyumba bora, salama na zenye gharama nafuu.
Waziri Akwilapo alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi NHC, akisisitiza kuwa utafiti wa kina ni nyenzo muhimu ya kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora, sambamba na kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Alieleza kuwa kupitia tafiti za kisayansi na matumizi ya teknolojia bunifu, NHC itaweza kubuni aina za nyumba na mifumo ya ujenzi inayozingatia uwezo wa kiuchumi wa wananchi, mazingira na upatikanaji wa vifaa vya ujenzi. Aidha, alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za NHC katika utafiti na maendeleo kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, wataalam na wadau wa sekta binafsi.
Katika ziara hiyo, Waziri Akwilapo aliipongeza menejimenti na wafanyakazi wa NHC kwa mchango wao katika utekelezaji wa agenda ya Serikali ya makazi bora, akibainisha kuwa mafanikio ya Shirika yanaakisi weledi, uwajibikaji na uzalendo wa watumishi wake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewataka wafanyakazi wa NHC kuwa mfano bora wa kuishi katika nyumba bora, ikiwemo kujenga au kumiliki nyumba zao binafsi, ili kuonesha kwa vitendo dhamira ya makazi bora na kujimudu kiuchumi.
Mmuya alisisitiza kuwa wafanyakazi wa NHC wanapaswa kuwa kielelezo cha mafanikio ya sera za makazi, akieleza kuwa haitarajiwa kuona watumishi wa Shirika wakijihusisha na tabia zisizoendana na hadhi na dhamana waliyonayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alimhakikishia Waziri kuwa Shirika litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kuzingatia sera za Serikali na kuhakikisha miradi yote inanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni