Princess of Pop, Britney Spears, ameuza katalogi yake yote ya muziki iliyodumu kwa zaidi ya miaka 27 kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 200, sawa na takribani shilingi za Kitanzania bilioni 516.
Taarifa zinaeleza kuwa mauzo hayo yalikamilika Desemba 30, 2025, ambapo haki hizo za muziki zimechukuliwa na kampuni ya uchapishaji wa muziki ya Primary Wave. Kupitia makubaliano hayo, Primary Wave itakuwa na umiliki wa sehemu kubwa ya nyimbo za Britney, hatua inayowapa udhibiti wa matumizi na mapato yanayotokana na kazi zake nyingi maarufu.
Britney Spears, ambaye amewahi kutamba na vibao kama …Baby One More Time, Toxic na Oops!… I Did It Again, anaungana na orodha ya wasanii wakubwa duniani walioamua kuuza katalogi zao za muziki kwa thamani kubwa katika miaka ya karibuni.
Kwa mujibu wa meneja wake, Cade Hudson, Britney amefurahishwa na uamuzi huo na ameusherehekea, akieleza kuwa thamani ya kazi zake imepata kutambuliwa ipasavyo.
Hatua hiyo inaonekana kama mkakati wa kifedha unaoweza kumpa uhakika wa mapato ya muda mrefu, huku mashabiki wakisubiri kuona ni mwelekeo gani mpya atakaouchukua katika safari yake ya muziki.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni