Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na World Health Organization (WHO) – Idara ya Dharura na Maafa, pamoja na wadau kutoka taasisi za serikali na binafsi, imeweka mikakati madhubuti ya kufanya tathmini ya athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura katika mkoa wa Dodoma.
Kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dodoma kimewakutanisha wataalamu wa sekta mbalimbali kwa lengo la kuchambua kwa kina changamoto za kiafya zinazotokana na majanga kama mafuriko, ukame, ajali za barabarani, milipuko ya magonjwa pamoja na majanga ya moto.
Kujenga Ustahimilivu Kabla na Baada ya Janga
Katika mjadala huo, washiriki wamejikita zaidi katika kuimarisha:
- Utayari wa sekta ya afya kukabiliana na majanga
- Uratibu wa wadau katika ngazi ya mkoa na taifa
- Elimu kwa jamii ili kupunguza athari kabla na baada ya majanga
Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha mifumo ya tahadhari na mwitikio wa haraka inaongezewa nguvu ili kupunguza madhara yanayoweza kuzuilika.
Mkoa wa Dodoma Watambua Changamoto Zake
Akifunga kikao kazi hicho Februari 13, 2026, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Charles Mduma, amesema kuwa Dodoma kama ilivyo kwa mikoa mingine, inakumbwa na athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura, hususan magonjwa ya mlipuko yanayochagizwa na ongezeko la idadi ya watu.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Mkoa ndiyo yenye jukumu la kuratibu masuala ya dharura na maafa, hivyo mafunzo na mpango kazi uliowekwa vitasaidia kufanya mapitio ya mipango ya mkoa, kuboresha maandalizi ya kifedha na kuhakikisha utekelezaji wa mikakati unafanyika kwa ufanisi.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, WHO pamoja na washiriki wote kwa kuandaa mpango kazi huo, akisisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu kwa watoa huduma za dharura na kamati za kukabiliana na maafa.
Kalenda Maalum ya Kutambua Nyakati Hatarishi
Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Udhibiti wa Athari na Majanga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. James Heller amesema kuwa kupitia mpango kazi huo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau itaandaa kalenda maalum itakayosaidia kubaini vipindi hatarishi mapema.
Kalenda hiyo, itakayojulikana kama Regional Risk Profile & Calendar, itawezesha:
- Kuchukua hatua za tahadhari mapema
- Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji
- Kupanga rasilimali kulingana na hatari zinazotarajiwa
Hatua hiyo inalenga kuifanya Dodoma kuwa miongoni mwa mikoa yenye mfumo thabiti wa maandalizi dhidi ya majanga.
WHO Yaahidi Kuendelea Kushirikiana na Serikali
Kwa upande wake, muwezeshaji kutoka WHO, Dkt. Pili Kimanga, amesema shirika hilo linaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kupunguza athari za kiafya zitokanazo na dharura.
Ameeleza kuwa msaada huo unahusisha:
- Kuimarisha uratibu wa sekta mbalimbali
- Kuboresha mifumo ya tahadhari mapema
- Kuunga mkono tathmini za kitaifa na mikakati ya afya
- Kuimarisha utayari wa vikosi vya tiba za dharura
- Kujenga uwezo wa kitaifa wa kukabiliana na majanga
Dhamira ya Utekelezaji
Kupitia azimio la kikao hicho, washiriki wanatarajiwa kurejea katika maeneo yao wakiwa na dhamira ya kutekeleza kwa vitendo mikakati iliyokubaliwa.
Hatua hii ni ishara kuwa mkoa wa Dodoma umejipanga si tu kukabiliana na majanga yanapotokea, bali pia kujenga mfumo wa tahadhari na utayari wa kudumu hatua muhimu katika kulinda afya na usalama wa wananchi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni