Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh, amekagua utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa gati la kuegeshea meli (floating jetty) unaotekelezwa na Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) katika Makao Makuu ya shirika hilo, Ras Mkwavi–Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo iliyofanyika Februari 10, 2026, ilimhusisha Prof. Sheikh kumwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Agness Meena. Katika ukaguzi huo, alijionea maendeleo ya mradi huo muhimu unaolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za uvuvi pamoja na kuboresha huduma kwa meli za uvuvi zitakazoendeshwa na TAFICO.
Akiwa katika eneo la mradi, Prof. Sheikh alimuelekeza mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Songoro Marine, kuhakikisha kazi zote zilizobaki zinakamilika na mradi kukabidhiwa ifikapo Februari 15, 2026, akisisitiza kuwa hakutakuwa na nyongeza ya muda hata kwa siku moja.
“Serikali imewekeza katika ujenzi wa miundombinu hii ili kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya uvuvi unakuwa madhubuti. Ni wajibu wa mkandarasi kukamilisha kazi kwa ubora na kwa wakati, hasa ikizingatiwa kuwa meli ya kwanza ya uvuvi inatarajiwa kuwasili nchini Februari 21, 2026,” alisema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Bi. Perpetua Massaga, akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, CPA Shaibu Matessa, aliishukuru Serikali kwa ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na shirika hilo.
Alisema ziara hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha miradi ya kimkakati inakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa sekta ya uvuvi pamoja na kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Buluu nchini.
“Shirika kupitia menejimenti yake litaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu ili ukamilike kwa mujibu wa mkataba na kuanza kutoa huduma stahiki mara moja,” alisema Bi. Massaga.
Mradi wa ukarabati wa gati hilo unatarajiwa kuongeza uwezo wa TAFICO kuhudumia meli za uvuvi kwa ufanisi zaidi, hatua inayotajwa kuwa chachu ya kukuza sekta ya uvuvi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni