Mvutano umeongezeka Mashariki ya Kati baada ya Marekani na Israel kuanzisha kile kilichoelezwa kuwa mashambulizi makubwa dhidi ya Iran huku Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kuanza kwa “operesheni kubwa za kijeshi” dhidi ya Tehran, akisema hatua hiyo inafuatia mashambulizi ya awali ya Israel.
Serikali ya Israel chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilieleza kuwa ilifanya mashambulizi ya “kujilinda mapema” dhidi ya malengo ya Iran wakati yenyewe Iran ilirusha makombora kuelekea Israel na pia kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Ghuba.
Miongoni mwa malengo yaliyotajwa ni Makao Makuu ya Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Bahrain.
Moshi ulionekana ukifuka katika maeneo kadhaa huku ripoti zikieleza kuwepo kwa milipuko karibu na vituo vya kijeshi vya Marekani katika ukanda huo.
Wakati huo huo, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amelaani shambulizi la anga lililopiga shule ya wasichana kusini mwa Iran, akilitaja kuwa “kitendo cha kinyama.” Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, idadi ya waliouawa imeendelea kuongezeka, huku Shirika la Habari la IRNA likiripoti vifo vya watu wasiopungua 57 na majeruhi 45.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni