Breaking


Jumatano, 25 Februari 2026

KARIAKOO KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA AFYA, JKCI YAFUNGUA KLINIKI YA MOYO


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI, imefungua kliniki mpya katika eneo la Soko Kuu la Kariakoo, Jijini Dar es salaam, hatua inayolenga kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya Moyo karibu na wafanyabiashara na wananchi.

Kliniki hiyo imeanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya Moyo bure kwa siku saba kwa wananchi watakaotembelea kabla ya kuendelea na utoaji wa huduma kwa utaratibu uliopangwa.


Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dokta Peter Kisenge, amesema kliniki hiyo imewekewa vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni-1 vikiwemo vinavyotumia teknolojia ya kisasa kuchunguza na kugundua magonjwa katika hatua mbalimbali.

Lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha watu wenye vipato vya aina zote wanapata huduma kwa urahisi, kwani JKCI inafuata kauli mbiu ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, ya Kazi na Utu, hivyo inajali utu wa watu.

Kliniki hiyo itakuwa na dawati maalum kwa wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali wanaofika Kariakoo, hivyo wasisite kupata huduma katika kliniki hiyo.

Naye, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Ashraph Abdulkarim, ameishukuru JKCI kwa kusogeza huduma za kibingwa Kariakoo na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kupima afya zao mara kwa mara.

Akitoa shukrani Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi, amesema uwepo wa kliniki hiyo ni msaada kwa eneo hilo ambalo hupokea zaidi ya watu laki moja kwa siku, ambalo awali halikuwa na huduma ya karibu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo.

Hakuna maoni: