Breaking


Jumanne, 10 Februari 2026

KENYA KUZUNGUMZA NA URUSI KUHUSU RAIA WAKE KUSHAWISHIWA KUPIGANA VITA UKRAINE

 


Serikali ya Kenya imetangaza mpango wa kuzungumza na Urusi kufuatia kuongezeka kwa ripoti zinazoeleza kuwa raia wake wanashawishiwa na kusajiliwa kwenda kupigana vita nchini Ukraine, hali ambayo Nairobi imeielezea kuwa haikubaliki kabisa.


Hatua hiyo inakuja wakati shinikizo likizidi kuongezeka kwa serikali ya Kenya kuchukua msimamo mkali, baada ya kugunduliwa kwa miili ya raia wake waliodaiwa kujiunga na vikosi vya jeshi la Urusi kupigana dhidi ya Ukraine.


Kwa mujibu wa mamlaka za Kenya, raia wanane waliokuwa wamesafiri hadi Urusi wamefariki dunia au hawajulikani walipo, huku kukiwa na taarifa kuwa bado kuna idadi nyingine ya raia wanaendelea kujiunga na kampeni hiyo ya usajili.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema mazungumzo kati ya Kenya na Urusi yatalenga kudhibiti na kupunguza vitendo vya kusajili raia kinyume cha sheria. Amesema pia majadiliano hayo yatahusisha masuala ya utoaji wa visa pamoja na mapitio ya makubaliano ya ajira kati ya nchi hizo mbili.


Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa inalinda haki, usalama na maisha ya raia wake popote walipo, huku ikiendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo linalozua wasiwasi mkubwa kitaifa na kimataifa.


Hakuna maoni: