Breaking


Alhamisi, 26 Februari 2026

KITONGA KUWA NJIA NNE, LENGO KUPUNGUZA FOLENI, USALAMA


Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa barabara ya Kitonga, Mkoani Iringa ambayo sasa itakuwa ya njia nne na yenye taa za barabarani. 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa hatua hiyo ni uamuzi wa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, ili kupunguza foleni na kuboresha usalama wa watumiaji barabara katika njia hiyo inayotumiwa na magari mengi. 

Waziri Ulega aliyekuwa katika ziara ya ukaguzi wa eneo la zaidi ya kilomita 7 linalopaswa kupanuliwa, amesema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa nchi kwa sababu inatumiwa pia na magari yanayokwenda katika nchi zinazotumia bandari ya Dar es Salaam kubeba mizigo yao. 

Akitoa picha ya ongezeko la uhitaji wa upanuzi wa barabara hiyo, amesema idadi ya magari yanayopita katika barabara kuu ya TANZAM, imeongezeka kutoka magari 1,700 hadi 3,400 kwa siku, hali inayopelekea barabara hiyo kuzidiwa na wingi wa magari.

Naye, Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, amesema barabara hiyo ni ya uchumi wa kimataifa, hivyo ikitengenezwa itainua zaidi uchumi wa mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla na kuwasaidia wananchi ambao hupata changamoto ya kufuata huduma za kijamii ikiwemo matibabu Iringa mjini. 

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADs, Mkoa wa Iringa, Yudas Msangi, amesema gharama ya upanuzi wa kilometa 7 wa njia mbili katika barabara hiyo ni Bilioni-59.2 na ukarabati wa njia mbili zilizopo ni Bilioni-16.2.

Hakuna maoni: