Serikali imesema itaendelea kuimarisha malezi ya watoto na utoaji wa mafunzo ya ustawi wa jamii kwa wananchi ili kupunguza changamoto za misongo ya mawazo, migogoro ya kifamilia na matatizo ya kisaikolojia, sambamba na kujenga jamii yenye maadili mema, ustawi imara na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hiyo katika kutoa wataalamu na elimu kwa jamii kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya watoto pamoja na ustawi wa familia. Amesema hali hiyo inachangia kujenga jamii yenye utulivu na maendeleo endelevu.
“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika eneo la malezi ya watoto na utoaji wa elimu ya ustawi wa jamii kwa wananchi kwa sababu tunaamini kuwa familia imara ndiyo msingi wa jamii imara. Kupitia mafunzo haya tunalenga kupunguza misongo ya mawazo, kuimarisha afya ya akili na kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye maadili mema.” alisema Mahundi.
Aidha, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ustawi wa jamii ili watoe huduma bora zinazokidhi mahitaji ya jamii na kusaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika familia na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Mwanga Mpapalike Mfaume amepongeza mchango wa Taasisi hiyo katika kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi, akisema hatua hiyo imekuwa na manufaa makubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii na kusaidia kupunguza changamoto za kijamii katika wilaya hiyo.
“Tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu na Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara ili kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kupata elimu na huduma za ustawi wa jamii, kwa kuwa tunaamini taasisi hii ni nguzo muhimu katika kusaidia kujenga jamii yenye ustawi, maadili mema na maendeleo endelevu,” alisema Mpapalike
Awali, akisoma taarifa ya Taasisi hiyo Meneja wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara Dkt. Leah Mwaisango amesema chuo kinaendelea kutoa mafunzo ya ngazi mbalimbali za taaluma ya ustawi wa jamii pamoja na mafunzo maalum kwa jamii, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa masuala ya malezi, makuzi ya watoto, ustawi wa familia na huduma za kijamii ili kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo.
“Taasisi imeendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa mafunzo kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, lengo likiwa ni kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kukabiliana na changamoto za kijamii, kuimarisha malezi ya watoto na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Leah.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha taasisi zake na kuhakikisha zinaendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa jamii, malezi bora ya watoto na afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata elimu na huduma zinazowawezesha kuishi maisha yenye ustawi na tija.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni