Breaking


Alhamisi, 26 Februari 2026

MSUKUMO MPYA KUKABILIANA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA, JKCI NA ABC GROUP KUSHIRIKIANA

 


Msukumo mpya katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza-NCDs unaendelea kushika kasi, ambapo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI, kwa kushirikiana na kampuni ya ABC Group, wamekubaliana kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya Moyo kwa wananchi.

Ushirikiano kati ya JKCI na ABC Group unatarajiwa kuongeza mwamko wa jamii kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuchukua hatua za mapema dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya Moyo.

Aidha, utafanyika kupitia wateja watakaonunua vifaa vya ujenzi katika kampuni ya ABC Group inayojuhusisha na usambazaji wa vifaa vya ujenzi, kupewa vocha yenye punguzo la asilimia 20 kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dokta Peter Kisenge, amesema Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza adhma yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo kwa urahisi zaidi.

Aidha, Dokta Kisenge, ametoa wito kwa kampuni na Taasisi nyingine kuungana na JKCI katika juhudi za kuielimisha jamii kuhusu kinga na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kama alivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mkurugenzi wa kampuni ya ABC Group, Mohammad Shareef, ameishukuru JKCI kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo na kuishirikisha katika masuala ya kufikisha huduma za afya katika jamii.

Magonjwa Yasiyoambukiza-NCDs yanayosababishwa na mchanganyiko wa vinasaba, mazingira, na tabia, yakiwemo magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, na magonjwa ya mapafu. 

NCDs husababisha asilimia 75 ya vifo duniani, vikiwa na hatari kubwa kutokana na uvutaji tumbaku, pombe, ulaji mbaya, na kukosa mazoezi.

Hakuna maoni: