Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imepokea msaada wa Point of Care Ultrasound Machine kutoka kampuni ya vifaa tiba ya Anudha, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za matibabu kwa watoto wachanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashine hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi ameeleza kuwa kifaa hicho kitakuwa msaada mkubwa katika kuongeza kasi ya utambuzi wa matatizo mbalimbali ya kiafya kwa watoto wachanga.
Mashine hiyo inaweza kufanya uchunguzi wa haraka na sahihi, hatua ambayo itawawezesha madaktari kufanya maamuzi ya kitaalamu kwa wakati na hivyo kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji uangalizi wa dharura.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Watoto, Dkt. Karungi Karoma, amesema Point of Care Ultrasound Machine
ina uwezo wa kupunguza muda unaoambatana na uchunguzi kwani matokeo hutolewa papo kwa hapo.
Amefafanua kuwa , kifaa hicho kinasaidia kupunguza uhitaji wa kumhamisha mtoto kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya vipimo, jambo ambalo kwa kawaida huongeza hatari kwa mtoto mwenye hali tete.
Naye Afisa Masoko wa Kampuni ya Anudha Bw. Tom Rweiza amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo za kushirikiana na Serikali na taasisi za afya kuboresha huduma za afya, hususan kwa makundi yenye uhitaji maalum kama watoto wachanga.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni