Timu ya mpira wa miguu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeibuka bingwa wa mchezo wa Mpira wa miguu katika Bonanza la michezo lililoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka liliofanyika tarehe 28 Februari, 2026 katika viwanja vya Kilimani, Jijini Dodoma.
Timu ya Mpira wa Miguu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imechukua ubingwa huo baada ya kuifunga timu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa magoli 5 kwa 4 katika changamoto ya mikwaju ya penati baada ya mchezo huo kumalizika kwa dakika 90 bila kufungana.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nahodha wa timu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Bw. Kanisius Ndunguru ameushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano wanaowapatia Watumishi wa Ofisi katika masuala ya michezo, huku akieleza kuwa ushindi huo ni zawadi kwa Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*“Tunaushukuru Uongozi kwa ushirikiano wanaotupatia, kwani wamekuwa wakituruhusu kushiriki katika matukio mbalimbali ya michezo.”* Amesema Bw. Ndunguru
Vilevile, Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliibuka washindi katika michezo mbalimbali ambapo Bw. Michael Mhina aliibuka mshindi katika mchezo wa kukimbia kwenye gunia, kukimbiza kuku Wanawake, Bi. Zela Rumanyila, kukimbia na yai kwenye kijiko Bi. Risper Washington, kukimbiza kuku Wanaume Bw. Lameck Makoye, kukaa kwenye kiti Wanawake Bi. Rehema Mgovano na kukaa kwenye kiti Wanaume Bw. Abdallah Hamza.
Kwa upande wake, Katibu wa Michezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Abdallah Hamza amewapongeza Watumishi wa Ofisi kwa kujitokeza na kushiriki katika bonanza hilo, huku akisisitiza umuhimu wa Watumishi kushiriki katika michezo katika kuboresha afya zao na kuimarisha ushrikiano baina yao.
Katika bonanza hilo, Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameshiriki kwa kufanya matembezi ya hiari kisha kufuatiwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kuvuta kamba, kufukuza kuku, riadha, kukimbia kwenye gunia, kukimbia na yai na kwenye kijiko.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni