Breaking


Jumapili, 8 Februari 2026

RAIS DK SAMIA AKEMEA UKIRITIMBA UGAWAJI VIZIMBA KARIAKOO.

Rais Dokta SAMIA SULUHU HASSAN, amesema kuzinduliwa kwa Soko jipya la Kariakoo, ni kufungua ukurasa mpya wa tumaini na nguzo kubwa ya shughuli za Kiuchumi kwa watanzania wengi wanaotegemea Biashara.

Amesema hayo leo wakati akifungua Soko Kuu Jipya la Kariakoo Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa ujenzi na upanuzi uliofanywa kufuatia janga la moto ulioteketeza Soko la awali mwezi Julai mwaka 2021.

Akizungumza Rais Dokta SAMIA ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, ihakikishe mchakato wa kuwarejesha Wafanyabiashara waliokuwepo awali, unafanyika bila kujuana, bila upendeleo, bila Ukiritimba na kusema asingependa kusikia wakubwa wanahodhi maeneo na kuwakodisha watu.

Rais amesisitiza Shirika la Masoko ndio likodishe Wafanyabiashara, na sio wakubwa wachukue maeneo na kuwakodisha Wafanyabiashara.

Aidha Rais ameelekeza Soko liwe na Kanzidata na kutaka ulipaji Kodi ufanyike kwa kutumia Mifumo na kuwepo uwazi kwenye Mapato na Matumizi.

Pia ametoa maelekezo kadhaa kuhusu Usalama wa Biashara na Wafanyabiashara na kusema ili Soko hilo liaminiwe Kitaifa na Kimataifa, ni lazima kuhakikisha Sokoni hapo panakua salama.

Rais Dokta SAMIA amesema Wafanyabiashara na bidhaa zao wanahitaji kuwa salama usiku na mchana, hivyo ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha suala hilo.

Pia amezungumzia usalama wa bidhaa zinazofikishwa Sokoni hapo na ametaka Mamlaka zote zinazohusika kusimamia bidhaa zinazoingia Sokoni.

Ameagiza kujengwe eneo la kulea Watoto ambalo litawekwa huduma za watoto ambao Wazazi wao watakua wanafanya shughuli zao Sokoni hapo.

Hakuna maoni: