Breaking


Ijumaa, 20 Februari 2026

RAIS SAMIA ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA KARDINALI PENGO

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa'ichi, kufuatia kifo Cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


Kupitia taarifa iliyotolewa leo Februari 20, 2026 na Ikulu, imeeleza kuwa Rais Dkt Samia amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Kardinali Pengo kilichotokea usiku wa jana Alhamis Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.


Rais Dkt Samia amesema anamkumbuka Kardinali Pengo kama kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.


Aidha Rais Dkt Samia amesema anaungana na Kanisa, waumini na Watanzania wote kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi na kumuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahala pema peponi.

Hakuna maoni: