Breaking


Jumanne, 3 Februari 2026

SERIKALI YATENGA BILIONI 7 KUWAWEZESHA VIJANA KATIKA UFUGAJI WA SAMAKI

 



Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga jumla ya shilingi bilioni 7 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu, ili kukuza sekta ya ufugaji wa samaki nchini.


Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Februari 3, 2026, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani, alisema fedha hizo zitanufaisha vijana 308 waliopatiwa mafunzo ya ufugaji wa samaki, hususan katika ufugaji wa samaki wa vizimba.


Mhe. Kamani alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Mhe. Dkt. Jasson Samson Rwekiza, aliyetaka kufahamu hatua za Serikali kuhusu utoaji wa mikopo ya vizimba vya samaki kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi.


Amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo, Serikali ilitoa mikopo ya vizimba 44 vyenye thamani ya shilingi milioni 986.80 katika Mkoa wa Kagera, ambapo wanufaika 101 walinufaika na mikopo hiyo.


Aidha, Naibu Waziri huyo alisema Serikali imeanza utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vizimba ndani ya siku 100, hatua itakayoongeza fursa za ajira na kipato kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Bukoba na Musoma.


“Serikali imetoa mikopo ya vizimba 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.126 kwa wafugaji wa samaki wa vizimba Musoma Mjini, ambapo wanufaika 130, wengi wao wakiwa vijana, walipata mikopo hiyo bila riba,” alisema Mhe. Kamani.


Aliongeza kuwa Wizara inaendelea kutekeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT–Uvuvi) kwa kutoa mafunzo ya vitendo na mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana, ili kuongeza uzalishaji, kipato na ajira katika sekta ya uvuvi.


Hata hivyo, Mhe. Kamani aliomba ridhaa ya Bunge kuendelea kutekeleza mpango wa kutenga asilimia 10 ya mikopo ya uvuvi kwa ajili ya ufugaji wa samaki wa vizimba katika maeneo yenye fursa, sambamba na juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuongeza idadi ya wanufaika nchini.


Hakuna maoni: