Breaking


Jumanne, 3 Februari 2026

SOKO LA MADINI SINGIDA: MAPINDUZI MAKUBWA YAMEANZA KATIKA BIASHARA YA MADINI


Wadau wa sekta ya madini mkoani Singida wameshuhudia mapinduzi makubwa katika biashara ya madini baada ya kuanzishwa kwa Soko la Madini Singida, ambalo limeimarisha uwazi, haki, na ufanisi kupitia mfumo wa bei elekezi za kidigitali.

Akizungumza katika soko hilo, Mjiolojia Mbeleye David, Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa, amesema kuwa soko hili limeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini, likiwalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei.

“Kabla ya kuanzishwa kwa masoko haya, wachimbaji wadogo wangeweza kutoa kati ya gramu 100 hadi 200 pekee. Sasa, uzalishaji unafikia kilo 50 hadi 60 kwa wachimbaji wadogo, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la ufanisi na imani katika mfumo wetu,” amesema David.

Soko la Madini Singida limejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya X-Ray Fluorescence (XRF) kwa ajili ya kupima ubora wa madini. Mfumo huu una kuhakikisha madini yanauzwa kwa thamani halisi, huku ubao wa kidigitali ukionyesha bei elekezi za madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba, na fedha. Hii imeongeza uwazi na kupunguza mianya ya udanganyifu katika biashara ya madini.

David amesisitiza kuwa mfumo wa bei elekezi uliowekwa na Serikali ni muhimu kumlinda mchimbaji mdogo dhidi ya kuuza madini kwa bei duni, huku shughuli za uthaminishaji na utoaji wa vibali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi zikifanyika kwa wepesi na haraka zaidi.

Kwa upande wake, mfanyabiashara Abubakari Omary, amesema elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi ni muhimu ili kuepusha sintofahamu na migogoro katika biashara ya madini:

“Elimu ni msingi muhimu ili kila mdau aelewe haki na wajibu wake na kufanya biashara kwa kuzingatia bei halisi ya soko,” amesema Omary.

Aidha, mfumo mpya wa masoko ya madini unaowezesha wachimbaji wasio na leseni kujisajili na kuuza madini yao moja kwa moja umeondoa kikwazo kikubwa kilichokuwepo awali.

Kwa jumla, Soko la Madini Singida limejitambulisha kama kichocheo kikubwa cha maendeleo ya sekta ya madini mkoani humo, likiongeza uwazi, usalama, na mapato ya serikali kwa kudhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini.

Hakuna maoni: