Tanzania imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa inayojihusisha na ufuatiliaji na udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi pamoja na ufadhili wa silaha za maangamizi kuwa itaendelea kuimarisha na kuboresha mifumo yake ya udhibiti wa vitendo hivyo, sambamba na viwango vya kimataifa vya uadilifu wa kifedha.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Ubadilishaji wa Taarifa za Udhibiti wa Fedha Haramu Duniani wa Kikundi cha EGMONT, uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Mhandisi Munde alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kujenga mfumo imara wa kupambana na uhalifu wa kifedha, ikiwemo kuimarisha taasisi za udhibiti, mifumo ya kisheria, pamoja na ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Hatua hizo zimeiwezesha Tanzania kuondolewa katika orodha ya nchi zenye mapungufu katika udhibiti wa utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi, baada ya kutekeleza kwa mafanikio mpango wa hatua uliowekwa na Kikosi Kazi cha Kudhibiti Utakatishaji Fedha (FATF).
Alifafanua kuwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya (EU) kuiondoa Tanzania katika orodha ya nchi zenye hatari kubwa umefungua ukurasa mpya wa kuaminika kwa mfumo wa kifedha wa nchi, hali inayochochea ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji wa kigeni.
“Tunajivunia mafanikio haya ambayo ni matokeo ya uongozi thabiti wa Serikali, mageuzi ya kisheria, pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zetu za ndani na washirika wa maendeleo,” alisema Mhe. Mhandisi Munde.
Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama wa Kikundi cha EGMONT pamoja na makundi mengine ya kikanda ikiwemo Kikundi cha Afrika Mashariki na Kusini cha Kuzuia Utakasishaji Fedha (ESAAMLG), ili kuhakikisha mifumo ya ndani inaendana na viwango vya kimataifa.
“Uhalifu wa kifedha hauna mipaka. Hakuna nchi inayoweza kushinda vita hii peke yake. Ushirikiano wa kimataifa, kubadilishana taarifa na kufuatilia mienendo ya fedha ni msingi wa ushindi wetu wa pamoja,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mhandisi Munde alizishukuru taasisi mbalimbali za kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha uwezo wa Tanzania, zikiwemo Kitengo cha Hazina cha Uingereza (UK Treasury), Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Mfuko wa Umoja wa Ulaya wa Kuzuia Utakatishaji Fedha na Ufadhili wa Ugaidi (EU Global Facility), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na Benki ya Dunia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya EGMONT, Bi. Elżbieta Franków-Jaśkiewicz, alisema Tanzania imeonesha maendeleo makubwa katika ushirikiano wa kimataifa tangu ilipojiunga na Jumuiya ya EGMONT, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kulinda uadilifu wa mfumo wa kifedha wa ndani na duniani kwa ujumla.
Alisema EGMONT itaendelea kusaidia wanachama wake kwa kutoa majukwaa salama ya kubadilishana taarifa za kifedha, kuimarisha ujuzi wa kitaalamu, na kusaidia mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha, ufadhili wa ugaidi na makosa mengine ya kifedha.
“Tunafurahi sana kukaribishwa nchini Tanzania, nchi yenye nafasi muhimu ya kimkakati katika kuimarisha ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kusini, na inayoendelea kuonesha dhamira ya dhati katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha,” alisema Bi. Jaśkiewicz.
Naye Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Bw. Majaba Magana, alisema safari ya Tanzania katika kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi imekuwa ya hatua kwa hatua, ikianza na kuanzishwa kwa Kitengo cha Ujasusi wa Kifedha chini ya Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha.
Alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake, FIU imekuwa mhimili muhimu wa kupokea, kuchambua na kusambaza taarifa za miamala ya kifedha, jambo lililosaidia kuimarika kwa uchunguzi wa makosa ya jinai na mashauri yanayohusiana na uhalifu wa kifedha.
“Mageuzi ya kisheria, uimarishaji wa usimamizi unaozingatia tathmini ya hatari, pamoja na kuongezwa kwa uwezo wa kiutendaji yameleta matokeo chanya na yanayoonekana wazi,” alisema Bw. Magana.
Mkutano huo wa EGMONT uliwakutanisha zaidi ya wajumbe 400 kutoka nchi wanachama zaidi ya 182, wakibadilishana uzoefu, maarifa na taarifa za kifedha kwa lengo la kuimarisha mapambano ya kimataifa dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu, makosa ya msingi yanayohusiana na hayo, pamoja na ufadhili wa ugaidi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni