Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa juhudi zake za kuimarisha usalama wa usafiri majini pamoja na kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea kifedha.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso (Mb) wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyofanyika leo tarehe 15, Februari,2026 katika ofisi za TASAC jijini Dar Es Salaam, ameeleza kuridhishwa na utendaji wa shirika hilo ikiwemo kuongeza mapato, kutoa gawio Serikalini, na kuendelea na zoezi la kurasimisha bandari bubu 20 zilizopo katika maeneo ya bahari na maziwa makuu ya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema shirika hilo limejipanga kuongeza kasi ya ununuzi wa vifaa vya utafutaji na uokoaji pamoja na kuendeleza urasimishaji wa maeneo ya bahari na maziwa yanayotumika kwa shughuli za usafiri majini.
"Hatua hizi zinalenga kuhakikisha wananchi wanasafiri kwa usalama, uhakika na ufanisi zaidi", amesema Bw. Salum
Aidha, ameeleza kuwa TASAC imepokea maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ya Sekta ya Uchukuzi ya kuongeza na kuboresha vifaa vya kutekeleza majukumu ya udhibiti wa usalama wa usafiri majini, kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji, pamoja na kuharakisha mchakato wa kurasimisha bandari bubu nchini.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni